----------------------------------------------------------------------------------------------------------------
[ IJUE TEHAMA ][ KISWAHILI NA TEHAMA ]
[ IJUE TEHAMA ][ KISWAHILI NA TEHAMA ]
____________________________________________________________________________________
MAENDELEO YA KISWAHILI KATIKA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (TEHAMA)
Aritamba
Malagira
Chuo
Kikuu Cha Dar es Salaam
Ikisiri
Teknolojia
ya habari na mawasiliano imekuwa ikikua kila siku kutoka simu ya kukoroga hadi
simu ya mkononi, matumizi ya wavuti na nyinginezo nyingi, kwa kweli ni hatua
kubwa ya maendeleo katika teknolojia. Hivi sasa watu wanawasiliana ndani ya
sekunde chache kwa umbali wa kutoka bara hadi bara kupitia wavuti. Katika hali
kama hii lugha za ulimwengu nazo zimekuwa zikijitahidi kukabiliana na ukuaji
huu wa teknolojia kwa kutafuta istilahi mpya ili kuelezea dhana mpya za
kiteknolojia zinazoibuka. Katika harakati hizi, Kiswahili hakiko nyuma,
istilahi mpya za Kiswahili zimekuwa zikiundwa ili kukidhi haja ya kuwasiliana
kupitia Teknolojia ya habari na mawasiliano. Makala hii inalenga kuangalia
hatua iliyofikiwa na Kiswahili katika tasnia ya teknolojia ya habari na
mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuchunguza istilahi za ki-TEHAMA zinazotumika.
1.
Utangulizi
Teknolojia
ya habari na mawasiliano imekuwa kiungo muhimu sana katika maendeleo ya watu
duniani. Watu wamekuwa wakitumia teknolojia hii katika kufanya mawasiliano
muhimu, kufanya bishara na mambo mengine mengi yanayowanufaisha watu. Kompyuta/
Talakirishi ni moja ya kifaa kilicholeta mapinduzi katika TEHAMA kama asemavyo
Katambi (2011) “Kompyuta ama Tarakilishi katika lugha ya Kiswahili ni
kifaa ambacho kimebadilisha kabisa mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo
takribani sita iliyopita. Kutokana na kuwapo kifaa hiki dunia imejikuta katika
maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile katika historia ya kuwapo
kwake. Kifaa hiki kimeleta mabadiliko makubwa Sana katika maisha ya kawaida ya
binadamu. Kifaa hiki kimesababisha mambo mengi kufanyika katika hali ambayo
hakika isingewezekana au ambayo awali ingeonekana kama ya kufikirika!. Kompyuta
imeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi. Kompyuta imeifanya dunia kuwa Kama kijiji
kidogo ambacho unaweza kukizunguka katika muda mfupi Sana wa sekunde chache”.
Maneno haya ya Katambi yanaonesha ni jinsi gani kompyuta ilivyo muhimi katika
TEHAMA, mawasiliano yote ya teknolojia ya habari hufanywa kwa kutumia kompyuta,
mfano; matangazo ya redio na televisheni, magazeti na n.k huandaliwa kwa
kutumia kompyuta na kuwa tayari kwa ajili ya kupasha habari.
Makala
hii, kwa kuzingatia umuhimu wa TEHAMA katika dunia ya sasa imejikita katika
kuchunguza maendeleo ya Kiswahili katika uga wa habari na mawasiliano kwa
umahususi zaidi katika mawasiliano yanayohusisha matumizi ya kompyuta hususani
wavuti na programu nyingine za kompyuta. Tutaangalia umuhimu wa matumizi ya
Kiswahili katika TEHAMA, maendeleo yaliyofikiwa, changamoto na mwisho ni
hitimisho.
2.
Usuli
Neno
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ujumla wake hurejelea mifumo
yote ya kiteknolojia inayotumika kutengeneza, kuhifahdi, kuchakata na kutumia
habari katika mifumo yake tofautitofauti (data, picha, uwasilishaji wa
medianuwai na mifumo mingine mingi) na mabayo huwezesha, kurahisha na
kutegemeza mawasiliano. Kwa umahususi zaidi, TEHAMA inarejelea kukutana au
kuingiliana kwa mikroelektroniki, talakirishi na mawasiliano
ya kutumia redio, simu au televisheni ambavyo hufanya kuwezekana kwa data,
ikiwa ni pamoja na matini, video na ishara za video kuweza kusafirishwa mahali
popote duniani ambapo ishara za kidijitali huweza kupokelewa… (Howell na
Lundall, wakinukuliwa na Akinyi 2010). Kwa ujumla TEHAMA inahusu mambo mengi
sana, matumizi ya kompyuta, wavuti, matangazo ya redio na televisheni,
satelaiti, picha na mambo mengine mengi yafananayo na hayo hujumuishwa katika
teknolojia ya habari na mawasiliano.
2.1 Umuhimu wa TEHAMA katika maendeleo kwa ujumla
Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano kwa ujumla imechangia sehemu kubwa kuleta maendeleo
hasa katika kipindi hiki cha karne ya 21 ambapo utandawazi umeenea ulimwengu
mzima na kuifanya dunia kuwa kama kijiji ambapo watu huwasiliana na kufanya
kazi na biashara kwa pamoja kama wapo katika kijiji kimoja, mambo haya yote
yanafanikiwa kwa kuwezeshwa na TEHAMA. Kama asemavyo Kamau (2009) kuwa
ushirikiano wa kimataifa katika mambo kama vile siasa, biashara, uchumi ,
michezo n.k huwezeshwa na kurahisishwa na teknolojia ya habari na
mawasiliano (TEHAMA) ambayo imeuunganisha ulimwengu mzima kimawasiliano. Kwa
maelezo haya tunaweza kuona ni jinsi gani TEHAMA ilivyo kuwa muhimu
katika ulimwengu wa sasa.
Lugha
ni muhimu sana katika suala zima la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
hatuwezi kuhamisha maarifa yaliyopo katika teknolojia hii bila kutumia lugha na
kwa hiyo ili kuwapo na maendeleo endelevu kupitia TEHAMA ni lazima pia lugha
inayotumika kuhamisha maarifa ya teknolojia hii iwe inaleweka kwa watumiaji
husika. Hii itakuwa rahisi kwao kuilewa na kuitumia teknolojia hii vilivyo kwa
sababu lugha inayotumika ni lugha wanayoifahamu na ni lugha yao.
Kama
tujuavyo bara la Afrika halijaendelea sana kwa kiwango cha kuzalisha teknolojia
zitakazo kubalika katika masoko ya kimataifa kama yafanyavyo mabara mengine
hususani mabara ya Ulaya na Marekani, kwa hiyo kulingana na hali hii Afrika
imekuwa ikiingiza teknolojia za kigeni kutoka Mabara mengine hasa Marekani na
Ulaya, teknolojia hizi zimekuwa zikiingizwa kwa lugha za kigeni jambo ambalo
hufanya watumiaji wengi wa Waafrika kushindwa kumudu matumizi ya teknolojia
hizi kwa sababu hawajui lugha iliyotumiwa. Kwa mfano kompyuta zinazoingizwa
Afrika programu zake huwa zimeandikwa kwa lugha za kigeni hususani kiingereza,
watu mabao wataweza kuzitumia kwa urahisi ni wale ambao wanazijua lugha hizi
vilivyo na kuwaacha wale wasiojua wakiwa wameduwaa ambao kimsingi ni wengi
kuliko wale wanaojua. Kwa hiyo, ili kuondokana na tatizo hili, upo umuhimu
mkubwa wa kuziendeleza lugha za Kiafrika kiteknolojia. Suala hili ni la msingi
sana, kwani kwa kufanya hivi hatutakuwa tumeendeleza lugha tu bali pia tutakuwa
tumeindeleza jamii yetu kiteknolojia.
2.2
Kwa nini Kiswahili katika TEHAMA
Wataalam
wengi wanipigia upatu lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya utandawazi barani
Afrika, hii ni kwa sababu lugha ya Kiswahili imeendelea sana kuliko lugha
nyingine za Kiafrika na ndiyo lugha pekee iliyoonekana kuwa tayari kupokea kwa
haraka mabadiliko ya kiteknolojia yanayoibuka kila siku duniani. Kwa maana
kwamba lugha ya Kiswahili ina utajiri mwingi wa msamiati kiasi cha kukabiliana na
teknolojia za kigeni zinazoibuka bila matatizo yoyote. Kama asemavyo Kamau
(2009) “kwa vile utandawazi huhusika na uunganishaji wa mataifa mbalimbali,
basi Afrika yahitaji lugha moja yenye asili ya Kiafrika kama lugha ya kusambaza
utandawazi. Kwa sasa mfano mzuri wa lugha kama hii ni lugha ya Kiswahili. Lugha
hii ndio lugha kutoka barani Afrika ambayo ina matumizi mapana kuliko lugha
nyingine hapa barani na kwingineko”. Nukuu hii inatuonesha ni jinsi gani lugha
ya Kiswahili ilivyo muafaka katika suala zima la utandawazi wa Afrika. Kimsingi
utandawazi husambazwa kupitia lugha na teknolojia, kwa hiyo tunaweza kuona
jinsi lugha ilivyo chombo muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia na kwahiyo
Kiswahili kama lugha ya kiafrika ni muhimu iwe imejiendeleza na kujitosheleza
kiteknolojia kwaajili ya mahitaji ya watu wake.
Kutokana
na umuhimu wa TEHAMA kama ilivyofafanuliwa hapo juu na kutokana na
umuhimu wa lugha katika maendeleo ya kiteknolojia, tunaweza kuona jukumu la
lugha ya Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Lugha ya
Kiswahili imebeba jukumu kubwa la kuhakikisha wakazi wa Afrika Mashariki
wanaipata na kuitumia teknolojia mpya kwa lugha wanayoifahamu ambayo ni
Kiswahili. Kwa kufanya hivi matumizi ya teknolojia yataimarika katika ukanda
huu wa Afrika Mashariki. Kwa misingi hii naweza kusema ndio sababu pekee
iliyonisukuma kuichunguza lugha ya Kiswahili katika uwanja wa Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano.
3.
Hatua iliyofikiwa na lugha ya
Kiswahili katika TEHAMA
Kwa
kweli lugha ya Kiswahili imepiga hatuta kubwa sana katika Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano. Kama tulivyo kwisha kusema huko awali kwamba TEHAMA ina uwanja
mpana sana, tunapozungumzia TEHAMA tunazungumzia vitu vingi sana kama vile
matangazo ya redio na televisheni kwa namna yanavyofanywa, matumizi ya kopmyuta
kwa namna yake n.k. Katika makala hii tutajikita zaidi katika matumizi ya
kompyuta kwa namna yake, tutajikita hapa kwani hii ndio inaonekana kuwa
teknolojia mpya kabisa katika mazingira ya lugha ya Kiswahili na dhana mpya zinazidi
kuibuliwa kila siku katika matumizi ya kompyuta.
Kompyuta
kimekuwa kifaa muhimu sana katika shughuli nyingi za kimaendeleo, kwa kutumia
kompyuta watu wamekuwa wakifanya mambo chungu nzima na kwa urahisi sana. Bila
shaka umekwisha sikia kuwa unaweza kununua bidhaa kwa kutumia kompyuta ukiwa
nyumbani kwako bila ya hata kwenda huko sokoni au dukani. Bila shaka umekwisha
sikia kuwa mabenki, hospitali, taa za kuongozea magari barabarani, kamera za
usalama, ndege za abiria na kivita na hata lift unazopanda kila siku unapoingia
na kutoka ofisini katika jengo refu huendeshwa kwa msaada wa kompyuta. Bila
shaka umekwisha jionea mwenyewe au kusikia habari kama hizi. Umekwisha sikia
kuwa mtu anaweza kumchagua mgombea wa urais au ubunge kwa kutumia kompyuta! Haya
na mambo chungu nzima hufanyika kwa msaada wa kompyuta. Katika nchi
zilizoendelea matumizi ya kifaa hiki yanaendelea kushika hatamu kiasi kwamba
kila kitu sasa kinafanywa Kwa kutumia mashine zinazoongozwa kwa kompyuta.
Kwa
hiyo unaweza kuona ni jinsi gani matumizi ya kompyuta yalivyokuwa muhimu sana
katika maisha ya kila siku. Serikali za Jumuia ya Afika mashariki zimekuwa
zikisisitiza matumizi ya kompyuta kuanzia shule za awali, kwa kuzingatia kwamba
matumizi ya kompyuta yameongezeka sana katika ulimwengu wa sasa lakini
changamoto zinazoikabili progaramu hii imekuwa ni lugha ya kufundishia. Kwa
mfano Tanzania somo la TEHAMA linafundishwa kuanzia shule za msingi; shule za
msingi kwa Tanzania hutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia
na kwa kuwa programu za kompyuta zimeandikwa kwa kiingereza,
italazimika programu hizo zitafsriwe katika Kiswahili ili ufundishaji uweze
kuwa rahisi. Na hapa ndipo tunapata istilahi mpya za Kiswahili katika
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Licha
ya uhitaji wa kufundishwa somo la Kiswahili katika shule za awali lakini pia
makampuni makubwa yanayohusika na mawasiliano ya kompyuta yamekuwa yakitafuta
nija ya kujiimarisha kibishara katika maeneo mbalilimbali duniani. Mbinu moja
wapo amabyo wemekuwa wakiitumia ni kuhakikisha wateja wao wanapata huduma kwa
lugha yao. Kwa mfano kampuni ya Microsoft kwa mara ya kwanza kabisa katika
historia ilianzisha mradi wa kutafsiri program zake kwa Kiswahili. Kama
asemavyo King’ei (2010) “kampuni ya talakirishi iitwayo microsoft ilitekeleza
hatua ya kihistoria mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi maalumu
inayowawezesha watumiaji wa talakirishi kutumia lugha ya Kiswahili katika
mawasiliano yao yote kwa kompyuta. Programu hii mpya inamwezesha mtumiaji
kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza kutumia kompyuta na
kuwasiliana bila shida yoyote”.
Msanjila
na wenzake (2011) pia wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha
ingizwa katika mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na
mikrosofti. Wanaendelea kusema, kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii
maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa
Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Kwa
mujibu wa maelezo ya wataalamu hawa ni wazi kwamba mpaka sasa hivi Kiswahili
kinatumika katika baadhi ya mifumo ya kompyuta. Katika kufanikisha hili
ujanibishaji wa programu kadhaa za kompyuta ulifanyika. Kahigi (2007) anasema
“Mradi wa ujanibishaji wa Office 2003 na Windows XP kwa Kiswahili sanifu
ulitekelezwa katika kipindi 2004-2005. Malengo ya maradi yalikuwa: (1) kuandaa
istilahi za kompyuta kwa Kiingereza-Kiswahili, na (2) kutafsiri programu nne za
kawaida za Office (Outlook, Excel, Word na PowerPoint) na Windows XP”. Hii
inamaanisha kwamba programu hizi zinapatikana katika lugha ya Kiswahili. Hebu tuangalie
mifano ya istilahi kutoka katika programu hizi za Office 2003 na Windows XP
kama zilivyoorodheshwa na Kahigi, ni istilahi zaidi ya 600 lakini hapa
tutaangalia chache tu:
- Fikia Access
- Kibonye fikishi Access key
- Viziada Accessories
- Amilisha Activate
- Kirekebu Adapter
- Kihadharishi Alert box
- Program matumizi Application
- Makaaba Archive
- Vitome mchoro Bit map
- Kiashiri mada Book mark
- Sakura Browse
- Kisakuzi Browser
- Kwa kaida By default
- Msabidi Configuration
- Sabidi Configure
- Puna Crop
- Kielekezi Cursor
- Tanafsi Custom
- Pakua Download
- Kijachini Footer
- Nakala bayana Hard copy
- Kidakuzi Cookie
- Sanidi Install
- Kicharazio Keyboard
- Kiolezo Template
- Tafutatua Trouble-shoot
- Sanidua uninstall
- Sasaisha Update
- Kidhulishi Highlighter
- Kichapishi Printer
- Kingavirusi Antivirus
Hizi
ni baadhi tu ya istilahi kati ya nyingine nyingi zilizoundwa katika mradi wa
kujanibisha programu za office 2003 na Windows XP. Jitihada za kampuni ya Microsoft
hazikuishia hapo tu, mnao mwezi mei mwaka 2011 kampuni hii ilizindua
programu ya Windows 7 kwa Kiswahili, hatua hii imezidi kukiimarisha Kiswahili
katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Haya ni maendeleo makubwa katika
lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo sasa mtumiaji wa Kiswahili anachaguo la kufanya,
ama kuendelea kutumia programu hizi kwa lugha ya Kiingereza au kwa lugha ya
Kiswahili.
4.
Changamoto zinazoikabili lugha ya
Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Kila
jitihada zinazofanywa katika kufikia malengo fulani huwa hakukosi changamoto.
Katika jitihada za kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kiteknolojia kumetokea
changamoto nyingi, moja wapo iliyo kuu kabisa ni kwamba lugha ya Kiswahili
haimilikiwi na taifa lolote tajiri kwa hiyo katika harakatika za kuendeleza
inakumbana na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa fedha na hata utayari wa
viongozi wa kisiasa kukiendeleza Kiswahili ni mdogo sana, hata hivyo harakati
hizi zinapingwa na mataifa ambayo lugha zao zimeendelea sana kiteknolojia kwa
kuhofia kwamba zitafunikwa na matumizi ya Kiswahili. Wapo tayari kutoa misaada
ili kuendeleza lugha zao kukididimiza Kiswahili kitu ambacho kinafanya harakati
za kukiendeleza Kiswahili kuwa ngumu kwani nchi kinamozungumzwa Kiswahili
hazina pesa za kupambana na mataifa makubwa yanayopigia upatu lugha zao.
Kutokana
na sababu hizo, kasi ya uundaji wa istilahi za kiteknolojia imekuwa ndogo sana,
kwani kufanya hivyo pia kunahitaji pesa, na mara nyingi pesa zimekuwa
zikitolewa na wahisani au makampuni yanayohusika kitu kinachotokea mara moja
baada ya muda mrefu sana.
Pia,
viongozi wa serikali hawajatilia mkazo suala hili, hawajaona umuhimu wa
kukiendeleza Kiswahili kitenolojia. Nguvu zao nyingi wameziweka katika miradi
mingine ya kimaendeleo huku wakisahau kabisa kuwa Kiswahili pia kinahitaji
kwenda sambamba na maendeleo hayo. Kwa hiyo hii imekuwa ni changamoto katika
maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Kwa
kuwa istilahi hizi zimekuwa zikifanywa na watu tofautitofauti, ni muhimu
kuwapo na jopo maalumu la kusanifisha istilahi hizi kabla hazijasamabazwa. Kwa
kufanya hivi hakutakuwa na matumizi tofauti ya istilahi katika dhana moja. Hali
hii inajitokeza sana endapo uundaji wa istilahi utakuwa umefanywa katika
makundi tofauti.
Utayari
wa watumiaji; watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili wamekuwa wakilalamika
kuhusu kutumia programu za komyuta kwa lugha za Kiswahili. Madai yao ni kwamba
istilahi za Kiswahili ni ngumu sana na hivyo si rahisi kuzitumia, kwa mfano,
wengi wamezoea kusema password na kwa hiyo ukiwaambi kwamba password
kwa Kiswahili huitwa nywila au mouse inaitwa puku watabaki
wakikushangaa na watona kama unawapa kazi kubwa sana. Kwa hiyo hii nayo
inasabaisha matumizi ya Kiswahili katika vifaa vya kiteknolojia hususani
kompyuta kuwa hafifu.
5.
Hitimisho
Katika
makala hii tumeona TEHAMA ni kitu gani na umuhimu wake katika maisha ya kila
siku ya binadamu, tumeona umuhimu wa lugha za kiafrika kuendelezwa katika
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa umahususi zaidi tumeona jinsi Kiswahili
kilivyo muhimu zaidi katika uwanja wa maendeleo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano. Tumengalia pia maendeleo yaliyofikiwa na lugha ya Kiswahili katika
TEHAMA huku tukionesha baadhi ya istilahi za Kiswahili zinazotumika katika
matumizi ya kompyuta, pia tumeangalia changamotozinazo ikabili lugha ya
Kiswahili katika jitihada za kuiendeleza kiteknolojia. Sasa tuangalie
mapendekezo juu ya nini kifanyike ili kuhakikisha lugha ya Kiswahili inashika
hatamu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano:
Viongozi
wa ukanda wa Afrika Mashariki waungane kuhakikisha wanaunda sera nzuri kuhusiana
na maendeleo ya lugha ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na kuandaa mradi maalumu wa
kuunda istilahi mbalimbali za kiteknolojia, hii itasaidia lugha ya Kiswahili
kuimarika katika matumizi ya teknolojia. Pamoja na hilo pia itenge bajeti
maalumu kwa ajili ya kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuunda istilahi
za Kiswahili katika teknolojia zinazoibuka ili kuahakikisha wazungumzaji wa
lugha ya Kiswahili hawaachwi nyuma katika matumizi ya teknolojia mpya
ziibukazo.
Pia
kutokana na changamoto ya kutokuwapo na jopo maalumu la kuunda istilahi za
kiteknolojia pindi mradi kama huu unapotokea, hali hii imesababisha kuwapo kwa
istilahi ambazo hazijasanifishwa na pengine kuwapo na istilahi zaidi ya moja
inayorejelea dhana moja, hii ni kwa sababu miradi kama hii hufanywa na watu
tofautitofauti na pengine wataalamu hawa wana ujuzi katika lugha tu lakini
katika teknolojia hususani kompyuta hawana maarifa ya kutosha au hawana kabisa.
Katika hali kama hii ni vigumu kuunda istilahi zinazofanana au zinazobeba dhana
kamili kama ilivyokuwa ikikusudiwa katika lugha chanzi. Kwa hiyo katika uundaji
wa istilahi za kiteknolojia ni vema kuwepo na jopo maalumu amablo lina ujuzi wa
kutosha katika lugha na masuala ya kiteknolojia, hii itasaidia kutoa istilahi
nzuri na zinazoeleweka kwa urahisi kwa watumiaji.
Baada
ya kuundwa istilahi hizi inatakiwa zisambazwe kwa watumiaji kwa kiwango
kinachoridhisha ili waweze kujifunza na kuzifahamu na hatimaye kuzizoea katika
matumizi yao ya kila siku katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Nasema
hivi kwa saba usambazaji wa istilahi hizi umekuwa haufanywi kwa kiwango
kinachohitajika, na katika usambazaji, vyombo vya habari vipewe kipaumbele,
kwani istilahi hizi zikitumiwa na vyombo vya habari itakuwa rahisi sana
kwa watumiaji wengine kuzitumia.
Wazungumzaji
wa Kiswahili pia wawe tayari kutumia istilahi hizi au programu za Kiswahili
katika matumizi yao ya kopmyuta. Programu kadhaa za kompyuta zimejanibishwa kwa
Kiswahili lakini wazungumzaji wengi wa Kiswahili bado wanatumia programu
zilizoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, program ya Windows 7 inapatikana kwa
Kiswahili lakini nina wasiwasi kama miongoni mwetu kuna mtu hata mmoja
anayetumia Windows 7 ya Kiswahili. Kwa hiyo napendekeza kwenu suala hili, kwa
kuwa sisi tumejitoa kueneza na kuienzi lugha ya Kiswahili pia ni jukumu letu
kuchangamkia fursa kama hizi, tuwe wa kwanza kutumia programu kama hizi kwa
Kiswahili pindi zinapotokea, kwa kufanya hivi tutakuwa tunakienzi Kiswahili na
kukikuza kwani watu wanaotuzunguka watakapotuona tunatumia Windows ya
Kiswahili watashawishika na wao kuitumia, hivyo kwa njia hii tutakuwa
tumefanikiwa kukuza na kuienzi lugha ya Kiswahili.
Ninaamini
kila mmoja wetu ana ndoto za kuona lugha ya Kiswahili siku moja inakuwa
lugha ya bara zima la Afrika, kwa maana kwamba Kiswahili kinazumgumzwa kila
kona ya bara hili, basi kama ndio ndoto zetu sote hatuna budi kupigania
maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwa nguvu zetu zote, tukifanya hivi kwa pamoja
kwa kijishughulisha na masuala yanayohusika na Kiswahili, kwa kuandika, kufanya
utafiti katika Nyanja mbalimbali za lugha ya Kiswahili ndoto zetu zitatimia na
kumbukumbu zetu zitakumbukwa katika vizazi vinavyokuja kama anavyokumbukwa leo
hii Shaaban Robert. Ninaamini kuwa tunaweza!!
Marejeo
Akinyi,
J.J. (2010). Kiswahili usage in ICT in NEPAD secondary schools in Kenya. Katika
TheJournal
of Language, Technology & Entrepreneurship in Africa, Vol. 2.
No.1.
www.ajol.info/index.php/kcl/article/vieFile
Kahigi,
K.K (2007). Ujanibishaji wa office na windows xp kwa Kiswahili sanifu.
Katika
Kioo
cha Lugha juzuu la 5. Dar es salaam. TUKI.
Kamau,
S.N. (2009). Kiswahili, utandawazi na umoja wa Afrika. Katika journal of
language, technology& entrepreneurship in Africa vol.1.
www.ajol.info/index.php/kcl/article/vieFile
Katambi,
S (2011). Teknolojia ya Habari na Mawasilianao (TEHAMA). Dar es salaam:
Modecs
Solutions
King’ei,
K (2010). Misingi ya isimujamii. Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili.
Msanjila,Y.P,
Kihore,Y.M na D.P.B Massamba (2011). Isimujamii sekondari na vyuo.
Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Osborn,
D. Z. (2006). African Languages and Information and Communication
Technologies:
Literacy, Access, and the Future. Katika Selected
Proceedings of the 35th
Annual
Conference on African Linguistics, ed. John
Mugane et al., 86-93. Somerville,
MA:
Cascadilla Proceedings Project. www.lingref.com,
document #1299.
Osborn,
D. Z. (2010). African Languages in a Digital Age. Cape Town: HSRC Press.
CHUO
KIKUU CHA DAR ES SALAAM
TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI
IDARA YA LUGHA YA KISWAHILI NA ISIMU
KI113:MBINU ZA UTAFITI NA
UANDISHI WA TASNIFU KATIKA LUGHA NA FASIHI
RIPOTI
YA UTAFITI KUHUSU MBINU ZILIZOTUMIKA KATIKA UUNDAJI WA ISTILAHI
ZA KISWAHILI ZILIZOINGIZWA KATIKA MIFUMO YA MAWASILIANO YA KOMPYUTA: MIFANO
KUTOKA MFUMO WA KOMPYUTA WA LINUX.
JINA:
MALAGIRA ARITAMBA.
NAMBA YA
USAJILI: 2010-04-02466
MWALIMU
WA SOMO: E. MAHENGE NA DKT. G. MRIKARIA
SHUKRANI
Utafiti
huu umefanikiwa kwa jitihada kubwa za waalimu wangu wa somo.Napenda nimshukuru
kwa dhati mwalimu Elizabeth Mahenge kwa kutumia muda wake mwingi katika
kunielekeza na kurekebisha mada yangu ya utafiti.Namshukuru pia Mwalimu
G.Mrikaria kwa kututia moyo katika kufanikisha utafiti huu.
Vilevile
nawashukuru wanafunzi wenzangu kwa kunishauri na kunitia moyo katika kuendelea
na utafiti huu.Wanafunzi wafuatao wamekuwa mchango mkubwa katika kufanikisha
utafiti huu;Ally Laila,Thomas Edson,Ndumbaro Eric, Ndege Busalu pamoja na
Ntenga Elias.Nawashukuru pia Boniface Jacob na James Balele kwa utayari wao wa
kunisaidia kuchapa utafiti huu.Na mwisho nawashukuru wote walionisaidia kwa
namna moja ama nyingine,Mungu awabariki sana!
__________________________________________________________________________________
YALIYOMO
Sura ya kwanza:Utangulizi na Nadharia ya uundaji
istilahi…………………. 1
1.0 Utangulizi……………………………………………………………………………………1
1.1 Tatizo la utafiti……………………………………………………………………….3
1.2 Malengo ya utafiti…………………………………………………………………....3
1.3 Umuhimu wa utafiti…………………………………………………………………4
1.4 Dhana ya istilahi,linux na nadharia ya uundaji
istilahi……………………………4
Sura ya pili:Mapitio ya marejeo na mbinu za ukusanyaji
data………………..8
2.1 Mapitio ya marejeo………………………………………………………………………….8
2.2 Mbinuza ukusanyaji data
……………………………………………………………..10
Sura ya tatu:Uchambuzi wa data………………………………………………11
3.1 Utangulizi………………………………………………………………………………….11
3.2 Mbinu zilizotumika
katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika Linux………….11
3.3 Ubora na udhaifu
wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katka Linux…16
3.3.1 Ubora wa mbinu zilizotumika ……………………………………………………16
3.3.2 Udhaifu
wa mbinu zilizotumika…………………………………………………18
3.3.3 Mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili…………………………19
Sura ya nne:Muhtasari na Hitimisho…………………………………………..20
4.1 Matokeo ya utafiti kwa
muhtasari…………………………………………………………20
4.2 Hitimisho…………………………………………………………………………………….22
Marejeo
Viambatisho
___________________________________________________________________________________
SURA YA KWANZA
1.0 Utangulizi
Lugha
ni kielelezo cha maisha ya jamii kwani huenda sambamba na mabadiliko au
maendeleo katika jamii. Kila sekta ya jamii iwe
siasa,elimu,sayansi,teknolojia,utamaduni,dini,kilimo,uhandisi,sanaa,uchumi ama
biashara hubadilika kila mara .Uvumbuzi mpya kila mara huzua dhana mpya ambazo zinahitaji
maneno mapya kuzielezea(King’ei 2010)
King’ei(ameshatajwa)
anaendelea kusema kuwa ukuzaji wa msamiati na istilahi ni jambo la
kawaida katika kurekebisha lugha ili iweze kuambatana na wakati au iwe ya
kisasa. King’ei anaendelea kusema kuwa ukuzaji upya wa istilahi hufanyika kwa
sababu mbalimbali.Kwanza kabisa lugha sharti iweze kuelezea dhana mpya
zinazoingia katika jamii kutokana na mabadiliko katika jamii.Sababu ya pili ni
kwamba maana ya maneno yanayotumika katika lugha hupanuliwa ili kuchukua maana
mpya au pana kuliko ile ya awali.Sababu ya tatu ya kuwepo haja ya kustawisha
istilahi mpya katika lugha ni ile haja ya kufasiri maandishi kutoka lugha moja
hadi nyingine.
Msanjila
na wenzake (2011) wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha ingizwa
katika mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na
mikrosofti.Wanaendelea kusema,kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii
maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa
Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Pia
King’ei(ameshatajwa) anaelezea kuwa,kampuni ya talakirishi iitwayo microsoft
ilitekeleza hatua ya kihistoria mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi
maalumu inayo wawezesha watumiaji wa talakirishi kutumia lugha ya Kiswahili
katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta,anaendelea kusema,programu hii mpya
inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza
kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote.
Katika
mchakato wa kuziweka programu hizi katika Kiswahili, ilihitajika kuunda
istilahi za
Kiswahili
ili kukamilisha shughuli hii mbinu mbalimbali za uundaji istilahi zilitumika.
Katika
uundaji wa istilahi za Kiswahili kuna mbinu mbalimbali zinazotumika. Kwa mujibu
wa
Kiango(2004)
amebainisha mbinu za kuunda istilahi za Kiswahili kuwa ni pamoja
na:Kubuni,anasema,njia hii inaweza kutumika katika kukabili mazigira ya aina
mbili; kubuni msamiati ambao utataja mambo yaliyomo katika jamii ambayo
hayajapata msamiati wa Kiswahili. Pili ni kubuni msamiati ambao utataja mambo
kutoka nje ya jamii yenye msamiati wa kigeni, mbinu nyigine ni kukopa; kukopa
kwa kutohoa msamiati wa kigeni,kukopa kwa kutafsiri msamiati wa kigeni na
kukopa kwa kuingiza maneno ya kibantu na lahaja na njia nyingine ni ya
kufupisha maneno.
Kahigi
(2004) anasema mbinu za kuunda istilahi ni pamoja na: unyambulishaji;
unyambulishaji ni kupachika viambishi undaji ili kuunda neno lenye dhana na
muafaka. Mfano, modification→ukumushaji. Mbinu nyigine ni ukopaji; ukopaji ni
kuchukua neno kutoka lugha chanzi na kulitohoa ili likubaliane na taratibu za
kisarufi za lugha pokezi. Mbinu zingine zilizoainishwa na Kahigi ni: tafsiri
mkopo;ni aina ya tafsiri kutoka lugha chanzi ambayo ni ya moja kwa moja, mbinu
nyigine ni uundaji wa maneno mapya, mbinu hii huhusisha uundaji wa maneno mapya
ambayo yalikuwa hayapo kwenye lugha lengwa, mfano byte >
baiti, uambatani; ni uwekaji wa maneno mawili au zaidi yanayowakilisha dhana
moja, mfano magneticfield >ugasumaku, ufupishaji; hii ni mbinu ya
kufinyanza maneno na kupata neno moja, mfano, UWT(Umoja wa Wanawake Tanzania).
Mtafiti
mwingine ambaye ameelezea mbinu za uundaji istilahi ni Sewangi(2004) yeye
anasema mbinu za uundaji istilahi ni pamoja na: kutohoa,kwa mfano; computer
> kompyuta, program>programu, mbinu nyingine ni kubuni, kwa
mujibu wa Sewangi anasema, mbinu ya kubuni inaweza kufanywa kidhahania au kwa
kutumia vigezo mahususi. Kubuni istilahi kidhahania hutetewa
kwa hoja kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya istilahi na dhana inayo
bebwa, hivyo neno lolote laweza kuundwa na kupewa hadhi ya istilahi ya dhana
fulani. Njia mojawapo ya kuunda istilahi kidhahania ni kutumia fomula za
kompyuta ambapo maneno mengi yanaweza kuzalishwa na kupachikwa dhana mahususi
katika uwanja fulani wa maarifa. Njia ya kuunda istilahi kivigezo huweza
kufanywa kwa kutumia vigezo mahususi kama
vile
kazi, umbo au mwonekano wa kitu. Kwa mfano kwa kutumia kigezo cha kikazi kisawe
cha calculator kimebuniwa kuwa ni kikokotozi (kitu kinachofanya kazi ya kukokotoa),
kisawe cha data saver kimekuwa kihifadhi data (kitu kinachohifadhi data). Mbinu
nyingine iliyoainishwa na Sewangi ni mbinu ya kupanua maana ya maneno yaliyopo;
njia hii huchukua neno lenye maana ya jumla na kuliongezea maana ya kihistilahi
katika mazingira ya kitaalamu, kwa mfano neno kifaru ambalo maana yake ya jumla
ni mnyama lakini katika mazingira ya utaalamu wa kijeshi ni kisawe cha tank.
Kwa
kuzingatia maelezo ya wataalamu hawa kuna mbinu tofautitofauti za kuunda
istilahi. Kwa hiyo kutokana na kwaba kuna mbinu tofautitofauti za kuunda
istilahi,utafiti huu hulenga kubainisha mbinu zilizotumika katika kuunda
istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux.
1.1
Tatizo la utafiti
Kulingana
na tafiti za wataalamu hawa,wameelezea kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo ya
kompyuta ya linux na Microsoft,kwa mfano, Msanjila na wenzake
(2011) na King’ei (2010) wameelezea kuhusu hili. Vilevile wataalamu wengine
kama vile Kiango (2004), Sewangi (2004) na Kahig i(2004) wao wameainisha mbinu
mbalimbali za kuunda istilahi za Kiswahili. Kwa ujumla wataalamu hawa
hawajaonyesha mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili
zilizoingizwa katika mifumo ya mawasiliano ya kompyuta hususani mfumo wa
kompyuta wa linux, kwa hiyo utafiti huu hulenga kuziba pengo hili kwa
kuchunguza mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux.
1.2
Malengo ya utafiti
Malengo
ya utafiti huu yamegawanyika katika sehemu kuu mbili:
Lengo kuu na
Malengo mahususi
1.2.1
Lengo kuu
Lengo
kuu la utafiti huu ni kutaka kutalii istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika
mfumo wa mawasiliano ya kompyuta wa linux na kuainisha mbinu
zilizotumika kuunda istilahi hizo.
1.2.2
Malengo mahususi
Malengo
mahususi ya utafiti huu ni mawili, ambayo ni: kupambanua ubora na udhaifu wa
mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux
na kubainisha mbinu bora zaidi inayoweza kutumika katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili.
1.3
Umuhimu wa utafiti
Umuhimu
wa utafiti huu ni kwamba utasaidia kubainisha mbinu bora za uundaji wa istilahi
za Kiswahili. Vilevile utafiti huu utawasaidia watumiaji wa kompyuta wanaotumia
programu hii ya linux kwa Kiswahili kuelewa kwa urahisi istilahi zilizotumika
baada ya kubainisha mbinu zilizotumika katika kuunda istilahi hizo.
1.4
Dhana ya istilahi, linux na nadharia ya uundaji istilahi
Istilahi
ni dhana iliyofasiliwa na wataalamu
mbalimbali na wote wanakubaliana kuwa, istilahi ni msamiati utumikao katika
uwanja fulani maalumu wa lugha. Wataalamu wanaokubaliana na fasili hii ni
pamoja na King’ei(2010), Samson(1988) na Kiango(2004). Kwa hiyo kulingana na
fasili hii si kila msamiati ni istilahi bali msamiati huwa istilahi pale
unapotumika katika Nyanja maalumu za kitaaluma. Kila uwanja maalumu wa kitaaluma
huwa na msamiati wake ambao hauna maana nje ya taaluma hiyo wala haufahamiki
kwa wazungumzaji lugha wasiokuwa wataalamu wa lugha hiyo. Kwa mfano msamiti
unaotumika katika isimu,fasihi,teknolojia ya habari na mawasiliano na kadhalika
ni maalumu na hutumiwa na kueleweka tu na wataalamu wahusikao na nyaja husika.
Linux kwa mujibu wa Msanjila na
wenzake(2011) ni mfumo wa kompyuta huria unao ruhusu watu mbalimbali kuchangia
katika marekebisho na maendeleo yake. Kimsingi linux ni mfumo endeshi wa
kompyuta. Ni program katika kompyuta iayosaidia programu-tumizi na mtumiaji wa
kompyuta kufikia vifaa fulani katika kompyuta ili kufanya kazi iliyokusudiwa, linux
ni sawa na
program-tumizi
zingine kama vile windows (Linux.com).
Nadharia
ya uundaji istilahi hujumuisha
mambo kadhaa, kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko(2008) mambo hayo ni pamoja
na sababu za uundaji wa istilahi, njia au mbinu za uundaji istilahi,vyombo vya
uundaji istilahi na misingi ya uundaji istilahi.
Katika
sababu ya uundaji istilahi Tumbo-Masabo na Mwansoko wanasema kuwa, uundji wa
istilahi ni muhimu panapotokea haja ya kushughulikia nyanja ambazo zilikuwa
hazishughulikiwi kwa kutumia lugha fulani. Uundaji huo aghalabu hufanywa ili
kukidhi haja ya mawasiliano katika elimu ya juu, ufundi na utaalamu,na shughuli
zinazohusu serikali na teknolojia. Kwa hiyo nadharia ya uundaji istilahi
huambatana na sababu au haja fulani ya kufanya hivyo. Kwa mfano uundaji wa
istilahi za Kiswahili katika mfumo wa kompyuta wa linux umeambatana na
sababu kwamba, kuuweka mfumo huu wa kompyuta katika Kiswahili ili kusudi
watumiaji wa Kiswahili waweze kuutumia mfumo huu kwa lugha wanayo ifahamu.
Vyombo
vinavyohusika katika uundaji wa istilahi.
Katika
kutekeleza kazi ya kuunda istilahi vimewekwa vyombo maalumu vinavyo tekeleza
suala hili, kwa mfano Tanzania chombo kilchopewa jukumu hili na serikali ni
Barza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).
Vilevile
katika nadharia ya misingi ya uundaji istilahi huzingatia mambo yafuatayo:
·
Uundaji wa istilahi ni budi uanzie kwenye dhana.
·
Dhana hizo zieleweke kwa ukamilifu na uwazi.
·
Uhusiano baina ya dhana ndio uwe msingi wa uundaji wa
istilahi, istilahi kopwa zichukuliwe kama zilivyo katika umbo lake la asili kwa
kufanya marekebisho machache tu kulingana na sarufi na matamshi ya lugha
kopaji.
·
Istilahi inafaa ziwe fupi iwezekanavyo lakini zieleweke.
·
Istilahi ziwe na muundo unaoeleweka yaani zifuate mofolojia
ya lugha.
·
Uundaji wa istilahi kwa vifupisho na akronomia uepukwe hasa
kama istilahi kamili si ndefu sana.
·
Istilahi zisiwe na sinonimia au homonimia.
·
Istilahi ziundwe kwa njia ambayo itakuwa rahisi kuunda
istilahi nyingine kwa
mnyambuliko.
·
Istilahi zitolewe kufuatana na mfumo wa dhana yaani
ziainishwe kuliko kuandikwa kwa alfabeti.
·
Muundo wa istilahi udokeze maana yake kwa watumiaji wa lugha
husika. Kwa hiyo misingi hii haina budi kufuatwa katika mchakato wa uundaji
istilahi.
Nadharia
nyingine kama ilivyoainishwa na Tumbo-Masabo na Mwansoko(wameshatajwa) ni njia
za uundaji istilahi. Katika uundaji wa istilahi kuna njia kuu mbili ambazo
zinatumika zaidi, njia hizo ni pamoja na:
(i)
Kutafsiri hasa kutoka kwenye lugha zinazojulikana kuwa ni za
kimataifa kama vile Kifaransa, Kiingereza, Kihisipania.
(ii)
Kuunda istilahi kutokana na mifumo ya dhana.
Njia
ya kutafsiri hutumiwa sana na vyombo vingi vya uundaji istilahi kinyume na
misingi ya uundaji ambayo inasisitiza kuwa uundaji huo uanze na dhana, msingi
wa njia hii ni istilahi za lugha chasili ambazo aghalabu hupangwa kwa alfabeti.
Faida ya njia hii ni kwamba istilahi nyingi zinaweza kushughulikiwa kwa
muda mfupi pia istilahi za lugha lengwa huweza kutafsiriwa katika lugha za
kimataifa. Hata hivyo hasara ya njia hii ni kwamba kwa vile kila istilahi
hushughulikiwa peke yake, hali hii huweza kusababisha mtiririko wa mfumo wa
istilahi usio na ulingano.
Kahigi
(2004) anasema kuunda istilahi kutokana na mifumo ya kidhana ni kwamba istilahi
huundwa kufuatana na mifumo hiyo. Kwa mfano katika hisabati kuna mifumo ya
elimu-maumbo, elimu-namba, vipimo na kadhalika. Mathalani katika kuunda
istilahi za dhana ya pembe itabidi dhana zifuatazo zishughulikiwe zote kwa
pamoja: pembekali, pembenukta, pembetatu, pembemshabaha, pebemstari na
kadhalika. Faida ya mkabala huu ni kwamba mwishowe mifumo yote ya dhana huwa na
mtiririko wenye ulingano.
Katika
nadharia hii ya njia za uundaji istilahi mbinu mbalimbali hutumika, mbinu hizo
ni pamoja na:mwabatano; hii ninjia ya uundaji istilahi kwa kuambatanisha
maneno mawili au zaidi yaliyo
huru.
Mfano ; mbwa kichaa.
Mnyambuliko;ni uundaji wa neno jipya kwa
kuambatisha viambishi kewenye mzizi au shina la neno. Mfano;wekeza
> uwekezaji.
Muungano; hii mbinu ni sawa na mwambatano
isipokuwa katika muungano maneno mawili au zaidi huunganishwa ili kuunda neno
moja, mfano;kiini+macho > kiinimacho.
Kupanua
maana ya maneno; huu ni
mchakato ambapo neno lililopo kwenye lugha hupewa maana pana zaidi ya maana
yake ya awali. Mfano butu maana yake ya kawaida ni –sio kali,-sio kata. Maana
ya kihistilahi ni pembe ambayo ni zaidi ya nyuzi 90 na ndogo kuliko
nhyuzi180(hisabati).
Ufupisaji; ni mbinu ambayo inatumika
kufinyanza fungu la maneno ili kuunda neno moja,mfano; BAKITA (Baraza la
Kiswahili laTaifa).
Ukopaji; ni matumizi ya neno kutoka lahaja
ama lugha nyingine, aghalabu neno hilo hubadilishwa ili lishabihi muundo wa
lugha lengwa.
Tafsiri-sisisi; ni aina ya tafsiri kutoka lugha
chasili ambayo ni ya moja kwa moja. Mfasiri habadili lolote ila anahakikisha tu
tafsiri inakuwa sahihi kwa mujibu wa lugha lengwa. Kwa hiyo katika mchakato wa
uundaji wa istilahi za Kiswahili mbinu hizi hutumika.
SURA YA PILI
Mapitio ya marejeo na mbinu za
utafiti.
2.1
Mapitio ya Marejeo
Kutokana
na mabadiliko yanayotokea katika jamii wataalamu wameonesha umuhimu wa lugha
kuyakabili mabadiliko hayo. King’ei(2010) anasema lugha ni kielelezo cha maisha
ya jamii siasa, elimu, sayansi, teknolojia, utamaduni, dini, kilimo, uhandisi,
sanaa, uchumi ama biashara hubadilika kila mara, uvumbuzi mpya kila mara huzua
dhana mpya ambazo zinahitaji maneno mapya ya kuzielezea.
Kulingana
na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano,lugha ya Kiswahili haina budi
kuyakabili mazingira haya. King’ei(ameshatajwa) anaelezea hatua ya kihistoria
iliyochukuliwa na kampuni ya Microsoft mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi
maalumu inayowawezesha watumiaji wa kompyuta kutumia lugha ya Kiswahili katika
mawasiliano yao yote kwa kompyuta. Kwa maana kwamba katika programu hii mpya
inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza,
kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote kwa Kiswahili.
Mtafiti
mwingine ni Msanjila na wenzake(2011) wanasema hadi wakati huu lugha ya
Kiswahili imekwisha ingizwa kwenye mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi
na mikrosofti. Wanaendelea kusema kuingizwa kwa Kiswahili katika
mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta
kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Kimsingi
hatua ya kuingiza Kiswahili katika mifumo hii ya kompyuta ni hatua muhimu sana
katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, katika mchakato wa
kuiweka mifumo hii katika lugha ya Kiswahili ilihitajika kuundwa istilahi za
Kiswahili ili mifumo hii iwekwe katika Kiswahili. Katika kuunda istilahi za
Kiswahili mbinu mbalimbali hutumika, wataamu mbalimbali wamejadili kuhusu mbinu
hizo:
Tumbo-Masabo
na Mwansoko(2008) wanasema mbinu za uundaji istilahi ni pamoja na: Muungano
wa maneno, mfano; mwanaisimu, mwambatano wa maneno, mfano; nusu
kipenyo,
8
Unyambulishaji, mfano; ambisha >
uambishaji, upanuzi wa maana za maneno, uhulutishji, mfano;
kizigeu > kiziogeu, ukopaji (kukopa kutoka lugha za
kigeni, lugha za kibantu au lahaja) na tafsiri-sisisi (tafsiri mkopo),
mfano; measure of time > kipimo cha wakati.
King’ei(2010)
ameainisha mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa ni pamoja na uunganishaji
wa maneno, ukopaji, kutafsiri maneno ya kigeni, mbinu ya ufupishaji mfano;UKIMWI
(Upungufu wa Kinga Mwilini) na utohozi.
Kahigi
(2004) anasema mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili ni pamoja na:unyambulishi,
uambatani, uhulutishi, ufupishaji, utemaji, ukopaji, tafsiri mkopo na uundaji
wa maneno mapya kabisa.
Vilevile
Kiango (2004) ameanisha mbinu zifuatazo katika undaji wa istilahi za Kiswahili:
kubuni na kukopa (kutoka lugha za kigeni, lugha za kibantu na
lahaja).
Kwa
hiyo kulingana na wataalamu hawa tunaweza kuanisha mbinu za uundaji wa istilahi
za Kiswahili kuwa ni:
·
Unyambulishji
·
Muungano wa maneno
·
Mwambatano wa maneno
·
Ukopaji
·
Tafsiri mkopo(tafsiri sisisi)
·
Uhulutishaji
·
Ufipishaji
·
Utemaji
·
Upanuaji wa maana ya maneno yaliyopo na
·
Kubuni
Tafiti
za wataalamu hawa zina umuhimu mkubwa kwani zimesaidia kujua kuingizwa kwa
Kiswahili katika mifumo ya kompyuta ya linux na Microsoft na
vilevi zimetusaidia kujua mbinu za uundji istilahi za Kiswahili. Kwa hiyo
katika utafiti wetu tutabainisha mbinu zilizotumika
kuunda istilahi za
Kiswahili katika linux kati ya hizo zilizoainishwa na wataalamu hao
2.2
Mbinu za ukusanyaji data
Katika
utafiti huu mbinu iliyotumika ni moja, yaani mbinu ya kusoma marejeo mbalimbali
hii ni kwa kuwa utafiti huu ni wa kimakitaba. Mbinu hii imetumika katika
ukusanyaji wa data zinazohusu istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo
wa kompyuta wa linux, ambapo mbinu hii imetumika kwa kusoma marejeo
kwa njia ya wavuti na kukusanya istilahi za Kiswahili zilizokuwepo katika mfumo
wa kompyuta wa linux.
Mbinu
hii pia imetumika katika kukusanya data zinazohusu mbinu za uundaji istilahi za
Kiswahili. Kwa kusoma marejeo mbalimbali data zinazohusu mbinu za uundaji wa
istilahi za Kiswahili zilikusanywa.
Vilevile
mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu ubora na udhaifu na
udhaifu wa mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux.
Na pia mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu kubainisha
mbinu bora katika kuunda istilahi za Kiswahili.
Data katika utafiti huu zimekusanywa
kutoka faharasa ya teknolojia ya habari ya KILinux(KlnX) juzuu ya kwanza.
Faharasa hii inajumuisha orodha ya istilahi 700. Sampuli ya utafiti
huu inajumuisha istilahi 100. Sampuli hii imechukuliwa kinasibu
(kiholela) yaani hakuna mpangilo au utaratibu wowote maalumu uliofutwa katika
uchukuaji wa sampuli.
SURA YA TATU
Uchambuzi wa data
2.1
Utangulizi
Utafiti
huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili, sehemu ya kwanza inahusu
uchambuzi wa data zinazohusu mbinu zilizotumika katika uundaji wa
istilahi za Kiswahili katika linux na sehemu ya pili inahusu
kupambanua ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili
katika linux na kubainisha mbinu iliyo bora katika kuunda istilahi za
Kiswahili. Katika uchambuzi wa data hizi tutatumia nadharia ya uundaji istilahi
za Kiswahili ambayo imekwishaongelewa katika kipengele cha 1.4.
2.2
Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika
linux.
Mbinu
zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux ni kama
zilivyobainishwa hapa chini:
Unyambulishi; katika mbinu hii kitenzi kinaweza
kugeuzwa kikawa nomino au kivumishi kinaweza kugeuzwa kikawa kitenzi au au
nomino. Mbinu hii imetumika kwa kiasi kikubwa, mifano ifuatayo hudhihirisha
matumizi ya mbinu hii.
·
Accessing > ufikio (
viambishi u-i-o vimeambatiswa katika shina fika).
·
Accsess
> fikio (viambishi i-o vimenyambulishwa
katika shina fika )
·
Allocation
> utengaji (viambishi u-aji vimeambatishwa
katika shina tenga)
·
Bookmark link > alamisho
(viambishi ish-o vimeambatishwa katika shina alama).
·
Bookmark > alamisha(t)
(viambishi ish-a vimeambatishwa na kuunda kitezi alamisha)
·
Deleting > ufutaji
(viambishi u-aji vimeambatishwa katika kitenzi futa )
·
Deletion > mfuto
(viambishi m-o vimeambishwa katika kitenzi futa nakupata
neno
mfuto)
·
Input > ingizo
(kiambishi –o kimeambishwa katika shina ingiza na kuunda istilahi ingizo).
·
Interactive > wasilianifu (
kiambishi –ifu kimeambishwa katika shina wasiliana na kuunda neno wasilianifu).
·
Allocation(n) > mtengo
(viambishi m-o vimeambishwa katika shina tenga na kuunda nomino mtengo ikiwa na
dhana ya matokeo).
Mwabatano; hii ni njia inayotumika kwa
kuambatanisha maneno mawili au zaidi. Katika linux kuna istilahi zenye
mwambatano wa maneno mawili na mwambatano wa maneno matatu. Mifano ifuatayo
inadhihirisha matumizi ya mbinu hii:
·
Add-on help > msaada nyongeza
( yameambatishwa maneno msaada na nyongeza).
·
Alphabet text character >
kiwambo alfabeti (kiwambo + alfabeti).
·
Aperture value >
thamani upenyo (thamani + upenyo)
·
Background colour > rangi
usuli (rangi + usuli).
·
Block device
> kitunza data ( (ki)tunza + data).
·
Bullet list > orodha
tobwe (orodha + tobwe).
·
Composer >
programu tumizi (programu+ tumizi).
·
Configuration utility >
programu sanidi (programu + sanidi).
·
Checksum > namba
thibitishi (namba + thibitishi).
·
Encrypted >
msimbo fiche (msimbo + fiche).
Vilevile
kuna istilahi zilizoundwa kwa kuambatanisha maneno matatu. Mfano:
·
Encrypted text >
matini-msimbo fiche (matini + msimbo + fiche).
·
Full-screen mode >
modi-skrini nzima (modi + skrini + nzima).
·
Small caps
> herufi kubwa ndogo (herufi + kubwa +
ndogo)
·
Column spam >
upana-safu wima (upana + safu + wima).
·
Default search engine >
injini tafuti-msingi (injini + tafuti + msingi).
·
Com port (communication port) > mlango wa
mawasiliano(mlango+wa+mawasiliano).
Muungano; hii ni mbinu ya kuunganisha maneno
mawili au zaidi ili kupata neno moja mbinu hii pia imetumika kuunda istilahi za
Kiswahili katika linux. Mifano ifuatayo inabainisha
kutumika
kwa mbinu hii:
·
Anonymity > ufichojina
(uficho + jina).
·
Arccosine > kosinitao
(kosini + tao).
·
Backslashes > mkwajunyuma (
mkwaju + nyuma).
·
Data area >
eneodata (eneo + data).
·
Data bank > kanzidata
(kanzi + data).
·
Data base > kihifadhidata
( (ki)hifadhi + data).
·
Footnote >
tiniwayo (tini + wayo).
·
Hypertext > matinifora
(matini + fora).
·
Keybody >
baobonye (bao + bonye).
·
Newsgroup > kundihabari
(kundi + habari).
·
Spreadsheet > lahajedwari
(laha + jedwari).
Ukopaji; njia hii pia imetumika kuunda
isuilahi za Kiswahili katika linux. Mifano ifuatayo inaonyesha kutumika kwa
mbinu hii.
·
Account > akaunti
·
Adapter > adapta
·
Ampersand > ampasendi
·
Applet > apuleti
·
Autoformat > fomati
otomati
·
Baud
> baudi
·
Boolean > buleani
·
Buffer >
bafa
·
Cursor >
kasa
·
Daemon > dimoni
·
Dial > dayo
·
Digit > dijiti
·
Icon > ikon
·
Kilobyte >
kilobaiti
·
Pixels >
pisel
·
Printer > printa
Mbinu
hii ya ukopaji imetumika kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili zilizopo katika linux.
Mbinu
nyingine iliyotumika kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa istilahi za Kiswahili
katika linux ni mbinu ya tafsiri mkopo (tafsiri sisisi). Tafsiri mkopo
nitafsiri ya moja kwa moja kutoka lugha chanzi. Mifano ifuatayo inathibitisha
matumizi ya mbinu hii katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux.
·
Actions menu > menyu vitendo.
·
Address book > kitabu cha
anwani.
·
Alert me >
nitahadharishe.
·
Auto complete > kamilisha
kiotomati.
·
Boolean operations
> matendo buleani.
·
Certificate manager
> meneja ithibati.
·
Certificate viewer >
kionyeshi hati.
·
Chat group
> kundi sogozi.
·
Colour capability
> uwezo kirangi.
·
Connection failure
> unganisho shinde.
·
Control panel
> paneli dhibiti.
·
Country code
> msimbo nchi.
·
Device manager >
meneja vifaa.
·
Dialogue box
> kisanduku cha mawasiliano.
·
Drag and drop > kokota
na dondosha.
·
Eject
> fyatua.
·
Flow control
> udhibiti wa mtiririko.
·
Word processor >
kichakata matini.
·
Web master
> mtawala tovuti.
Mbinu
nyingine ni mbinu ya kuunda maneno mapya kabisa mbinu hii imetawaliwa na
maneno ya mkopo. Mfano:
·
Icon > ikoni
·
Italic > italiki
·
Label > lebo
·
Megabyte(MB) >
megabaiti(MB)
·
Menu proxies >
menyu proksi
·
Manager > meneja
·
Pixels > piseli
·
Program > programu
·
Scan > skani.
·
Scanner > skana
·
Tab > tabo
·
Tag > tagi
Mbinu
ya ufupishaji pia
imetumika katika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux; hii ni mbinu
inayotumika kufinyanza fungu la maneno na kupata neno moja. Mifano ifuatayo
huonyesha matumizi ya mbinu hii:
·
Alt(alternate) >
Kbdl (kibadala)
·
BSS (Bulletin Board Service)
> HUM (Huduma za Ubao wa
Matngazo)
·
Ctrl (ontrol) >
Kdbt (kidhibiti)
·
ESC (escape) > Epa
(epuka)
·
FAQ (frequently asked quetions)
> MYM (Maswali Yaulizwayo Mara kwa mara)
·
FTP (file transfer protocol)
> IKF (Itifaki ya Kuhawalisha Faili)
·
FYI (For Your Information)
> KTY (Kwa Taarifa Yako)
·
Megabyte (MB)
> megabaiti (MB)
·
Ref:
> Yah:
·
Re:
> Jb:
·
TCP (Transfer Control Protocol)
> IKU (Itifaki ya Kudhibiti Urushaji)
·
URL (Uniform Resource Location)
> KISARA (Kioneshi Sanifu Rasilimali)
·
WWW (World Wide Web)
> WWW (Wavu Wa Walimwengu)
Uhulutishi ni mbinu pia liyotumika katika uundaji
wa istilahi za Kiswahili katika linux, mbinu hii hutumika katika uundaji
wa istilahi kwa kuunganisha sehemu za maneno na kuunda neno moja. Mbinu hii
imetumika kwa kiasi kidogo sana, rejea mifano ifuatayo:
·
Bitmap > taswidoti (
(taswi)ra + doti)
·
Multimedia > medianuwai
((medi)a + anuwai)
Mbinu
nyingine iliyotumika katika uundaji wa istilahi za kiswahili katika linux
lakini kwa kiasi kidogo sana ni ile mbinu ya upanuzi wa maana za maneno,
upanuzi wa maana za maneno ni kuongezea maana maalumu za kihistilahi katika
maneno ya Kiswahili. Mfano:
·
Mouse
> puku
Puku
kwa maana ya kawaida ni panya pori lakini hapa limepewa dhana mahususi katika
kompyuta kwa maana ya kifaa kinachotumika katika utumiaji wa kompyuta.
Utemaji (clipping) ni mbinu pia
iliyojitokeza kwa kiasi kidogo sana, kwa kutumia mbinu hii istilahi huundwa kwa
kukata sehemu ya neno na sehemu ya neno itakayobaki hutumika kama istilahi.
Mfano: key (on keyboard) >
kibonye ( kutoka neno bonyeza na kuongeza kiambishi cha ngeli ya saba ki-).
Kwa
hiyo hizi ndizo mbinu zilizobainika kutumika katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux.
Ubora na udhaifu wa mbinu zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katika
linux.
2.3.1
Ubora wa mbinu zilizotumika.
Kwa
kiwango kikubwa mbinu zilizotumika zimezingatia misingi na kanuni za uundaji
istilahi. Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008) wanabainisha kuwa
misingi mahususi
katika
uundaji wa istilahi ni pamoja na: Uangavu wa wa istilahi iliyoundwa yaani
istilahi ziakisi sifa bainifu za dhana zinazoziwakilisha. Mbinu zilizotumika
katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux kwa kiasi kikubwa
zimezingatia msingi huu. Kwa mfano:
Ufikio
>
accessing, ingizo
> input,
alamisha > bookmark.
Istilahi
hizi zinaonyesha wazi dhana zinazowakilishwa, kwa mfano, alamisha inabeba dhana
ya kitendo cha kuweka alama hivyo kwa msingi huu inadhihirisha
mbinu zilzotumika ni bora. Vilevile mbinu zilizotumika zimezingatia msingi wa
uundaji istilahi unaosema, istilahi sharti ziwe na uwezo mkubwa wa kunyambuliwa
na kuunda istilahi nyingine za kikoa au ukanda unaohusika. Msingi huu umefuatwa
katika kuunda istilahi za kwenye linux, kwani istilahi nyingi
zilizoundwa zina uwezo wa kunyambulishwa. Mfano:
·
Add > ongeza
·
Add-on > nyongeza
·
Alert(n) >
thadhari
·
Alert(v) >
tahadharisha
Pia
uundaji wa istilahi za kwenye linux umezingatia msingi wa uundaji
istilahi unaosema,uwakilishi wa istilahi moja kwa dhana moja. Msingi huu
umezingatiwa kwa kiasi kikubwa kwani istilahi takribani zote huwakilisha dhana
moja isipokuwa zile zilizoundwa kwa kupanua maana ambazo ni chache sana.
Mfano:
configuration > usanidi
Configuration file > faili sanidi
Vilevile
mbinu zilizotumika ni bora kwani hazijatumia kwa kiasi kikubwa mbinu za
uhulutishi na mbinu ya kupanua maana ya maneno yaliyopo, hii ni kwa sababu
misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili husisitiza kuepuka matumizi ya
mbinu hizi; hii ni kwa kuwa istilahi zinazo uundwa kwa mbinu ya uhulutishi huwa
na uvulivuli wa maana na kufanya kuwa ngumu kukumbukwa na kutumiwa. Pia uundaji
wa istilahi kwa kupanua maana ya maneno yaliyopo husababisha watumiaji wa
istilahi hizi kushindwa kutofautisha maana zake za kawaida na zile za kihistilahi.
Mbinu
za uundaji istilahi za Kiswahili katika linux, pia zimezingatia msingi wa
uundaji wa istilahi za Kiswahili unaosema, istilahi sharti ziwe fupi na zenye
kueleweka. Istilahi nyingi zimeundwa kwa kuzingatia msingi huu.
2.3.2
Udhaifu wa mbinu zilizotumika
Katika
uundaji wa istilahi za Kiswahili za kwenye linux, kuna baadhi ya mbinu
zilizotumika zinazoonyesha kuvunja kanuni na misingi ya uundaji istilahi. Kwa
mfano kuna istilahi zilizoundwa kwa kukiuka msingi wa uundaji istilahi
unaosema, istilahi sharti ziwe fupi na zenye kueleweka. Kuna baadhi ya istilahi
ambazo ni ndefu na hivyo kukiuka huu msingi. Mfano:
·
Allow popup from this site
> ruhusu udukizi kutoka tovuti hii
·
Com port
> mlango wa mawasiliano
Istilahi
hizi zimeonekana kuwa ndefu kwa sababu mbinu iliyotumika ni ya mwambatano wa maneno,
na kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko wanasema, “iwapo istilahi zitaundwa
kwa kutumia mbinu za muungano na mwambatano wa maneno basi mambo yafuatayo
itabidi yazingatiwe”:
i.
Idadi ya maneno yanayounganishwa au yanayoambatanishwa
yafaa yasizidi mawili.
ii.
Vistari visitumike kutenga istilahi ambatani kwani katika
Kiswahili istilahi za namna hii hutamkwa kama neno moja lenye mkazo mkuu kwenye
silabi moja tu.
iii.
Istilahi za namna hii yafaa zisiwe na silabi zaidi ya nane
kwani kwa kawaida maneno ya Kiswahili yanawastani kati ya silabi moja na tano
tu. Kwa msingi huu mifano ya itilahi zilizotolewa hapo juu zimeundwa na maneno
zaidi ya mawili na silabi zaidi ya nane. Mfano ; mlango wa mawasiliano (silabi
10), ruhusu udukizi kutoka tovuti hii (silabi 15) na hivyo huu ni udhaifu
uliojitokeza.
Vilevile
matumizi ya mbinu za uhulutishi na upanuzi wa maana ya maneno yaliyopo
zimetumika, huu ni udhaifu kwani misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili
inasema, mbinu ya
uhulutishaji
iepukwe kwani etimolojia yake ina uvulivuli na uundaji wa istilahi kwa kupanua
maana ya maneno yaliyopo yafaa uepukwe kwani istilahi za namna hii
zinawakanganya wengi hasa zinapotumika nje ya muktadha au kwenye taaluma zenye
mahusiano ya karibu.
Mifano
ya istilahi zilizoundwa kwa uhulutishaji ni:
·
Taswidoti
> bitmap
·
Medianuwai
> multimedia
Na
mfano wa istilahi iliyoundwa kwa upanuzi wa maana ya neno ni:
Puku
> mouse. Puku ni istilahi iliyopanuliwa maana ambapo
maana yake ya kawaida ni panya pori lakini maana yake maalumu ni kifaa
kinachotumika katika utumiaji wa kompyuta.
Kwa
hiyo huu ndio udhaifu wa istilahi zilizotumika katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili katika linux.
2.3.3
Mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Kulingana
na utafiti huu mbinu zilizoonekana kuwa bora zaidi na ambazo zinatumika sana
katika uundaji wa istilahi za Kiswahili ni pamoja na, unyambulishaji, ukopaji,
mwambatano, muunganiko pamoja na tafsiri mkopo. Mbinu hizi zimeonekana kuwa
bora katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kwa sababu zinaruhusu uundaji
istilahi kwa wingi iwezekanavyo na mbinu hizi huzingatia misingi ya uundaji
istilahi za Kiswahili. Misingi hiyo ni pamoja na ufaavu wa kiisimu, uwekevu wa
kiisimu, unyambulifu , uwakilishi wa istilahi moja kwa dhana moja, udhahiri na
utoshelevu pamoja na uangavu. Mbinu hizi huakisi kwa kiasi kikubwa misingi hii
na hivyo kupendekezwa na waunda istilahi katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili.
SURA YA NNE
Muhtasri na Hitimisho
4.1
Matokeo ya utafiti kwa muhtasari
Utafiti
huu umeongelea malengo matatu. Kwanza utafiti huu umebainisha mbinu za uundaji
istilahi zilizotumika katika linux. Pili utafiti umepambanua ubora na udhaifu
wa mbinu za uundaji istilahi za Kiswahili zilizotumika katika linux. Tatu
umebainisha mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Utafiti
huu umeonyesha kuwa mbinu kumi za uundaji istilahi za Kiswahili zimetumika
katika istilahi za linux. Mbinu hizo ni pamoja na:
Unyambulishi; mifano ya istilahi zilizoundwa kwa
mbinu hii ni kama vile:
·
Ufikio > accessing
·
Utengaji > allocation
·
Alamisho > bookmark
link
·
Ingizo > input
Muungano
wa maneno; mifano ya istilahi
zilizoundwa kwa mbinu hii ni pamoja na:
·
Ufichojina > anonymity
·
Mkwajunyuma > backslashes
·
Kanzidata
> databank
Ukopaji; mbinu hii pia imetumika katika
kuunda istilahi za kwenye linux. Mfano:
·
Akaunti > account
·
Apuleti >
applet
·
Dayo
> dial
Tafsiri
mkopo (tafsiri sisisi);
mifano ya istilahi zilizoundwa kwa kutumia mbinu hii ni:
·
Menyu vitendo >
actions menu
·
Meneja ithibati >
certificate manager
·
Paneli dhibiti
> control panel
Mwambatano; mbinu hii vilevile
imebainishwa kutumika katka uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux:
Mifano:
Rangi usuli > background color
Orodha tobwe > bullet list
Thamani upenyo > aperture value
Kuunda
maneno mapya kabisa; mbinu
hii pia imetumika. Mfano.
·
Ikoni > icon
·
Italiki > italic
·
Menyu proksi > menu proxies
Ufupishaji; katika utafiti huu mbinu hii pia
imetumika. Mfano:
·
Kbdl (kibadala) > Alt
(alternative)
·
Kdbt (kidhibiti) > Ctrl
(control)
·
Epa (epuka)
> Esc (escape)
·
KISARA (Kioneshi Sanifu Rasilimali )
> URL (Uniform Resource Location)
Uhulutishi; mbinu hii pia imetumika. Mfano:
·
Taswidoti > bitmap
·
Medianuwai > multimedia
Upanuzi
wa maana; mfano, puku (panya
pori) > mouse.
Utemaji
(clipping); mbinu
hii pia imetumika. Mfano, kibonye > key (on
keybody).
Kwahiyo
hizi ndizo jumla ya mbinu zilizo tumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux.
Matokeo
ya utafiti huu yanaonyesha mbinu zilizotumika ni bora kwa kiasi kikubwa hii ni
kutokana na sababu kwamba, mbinu zilizotumika zimezingatia misingi na kanuni za
uundaji istilahi kwa kiasi kikubwa. Lakini vilevile baadhi ya mbinu za uundaji
istilahi zimetumika
ambazo
kwa mujibu wa misingi ya uundaji istilahi hazifai kutumiwa katika mchakato wa
uundaji wa istilahi za Kiswahili. Mbinu hizi ni pamoja na uhulutishi na upanuzi
wa maana ya maneno yaliyopo.
Pia
utafiti huu umebainisha mbinu bora katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa
ni unyambulishaji, muungano wa maneno, uambatishi, mkopo pamoja na tafsiri
mkopo. Hii ni kwa sababu mbinu hizi huzingatia misingi ya uundaji wa
istilahi za Kiswahili kwa kiwango kikubwa.
3.2
Hitimisho
Katika
mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili kuna misingi ambayo hainabudi
kufuatwa. Ili kuunda istilahi zilizobora mwanahistilahi hanabudi kuzingatia
misingi hii.
Kwa
mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008) wanasema kuwa ili kuinua ubora wa
istilahi za Kiswahili waundaji istilahi wanasisitizwa kuzingatia mambo matatu
muhimu. Kwanza wanasisitizwa kwa kadri iwezekanavyo wafuate kwa makini kanuni
na taratibu za uundaji istilahi za Kiswahili. Kwa kufanya hivi itawezesha kwa
kiwango kikubwa kuundwa istilahi za Kiswahili zenye kulandana vizuri kisarufi.
Pili
waundaji istilahi wanahimizwa kuachana na mtindo wa kuunda istilahi moja moja
kukidhi mahitaji yao ya istilahi ya papo kwa papo kwani mtindo huu unasababisha
uundaji wa istilahi zisizo na mtiririko na utimilifu wa kuridhisha. Kwa
kuwa dhana zinazo wakilishwa na istilahi kwa kawaida huwa hazikai pweke pweke
bali hukaa kama seti au mifumo maalumu, basi ni vema uundaji istilahi ufuate
vilevile mifumo hiyo ya kidhana. Kulingana na maelezo haya kinachosisitizwa ni
uundaji wa istilahi kwa kuzingatia mifumo ya kidhana. Kwa mujibu wa
Tumbo-Masabo na Mwansoko (wameshatajwa) wakimnukuu Mkude (1989:34) wanasema,
uundaji
wa istilahi kwa kuzingatia mfumo wa kidhana unafaida kuu nne:
(i)
Utawasaidia waunda istilahi kuonyesha wazi mantiki ya
uhusiano baina ya istilahi za ukanda mmoja.
(ii)
Utawahimiza waunda istilahi kubainisha vizuri zaidi tofauti
ndogondogo lakini muhimu baina ya istilahi zinazokaribiana.
(iii) Utawasaidia kutambua haraka mapengo katika nasaba au
upungufu katika maelezo.
(iv) Utawasaidia waunda istilahi kuona haraka ni istilahi zipi
zitaweza kuathiriwa upesi iwapo kutatokea mabadiliko katika istilahi moja
wapo.
Hivyo
utaratibu wa uundaji istilahi kinasaba ukitumiwa utaepusha uundaji wa istilahi
zinazogongana na zisizo na mtiririko wenye mantiki.
Jambo
la tatu kama ilvyoainishwa na Tumbo-Masabo na Mwansoko ni kwamba uundaji wa
istilahi haunabudi kuzingatia tofauti za watumiaji, mathalani viwango vyao vya
elimu, mazingira yao na kadhalika. Kwa hali hii ili kuhakikisha istilahi bora
za Kiswahili zinaundwa ni muhimu hadhira mahususi za watumiaji istilahi
ziainishwe na istilahi ziundwe kufuatana na viwango vya elimu ya watumiaji
lengwa. Ni kwa kufanya hivyo dhana kama vile istilahi angavu au istilahi zenye
uvulivuli zitakuwa na maana halisi kwani zitahusishwa na vikundi mahususi vya
watumiaji istilahi.
Na
Aritamba Malagira.
Haki
zote zimehifadhiwa.
MAREJEO
Kahigi,K.K
(2004).Ujanibishaji wa office na windows xp kwa Kiswahili sanifu katika
http//ajol.info.
Kiango,J.G
(2004). Uundaji wa msamiti mpya katika Kiswahili: Zoezi lenye njia
mbalimbali
katika Kiango.htm.
King’ei,
K (2010). Misingi ya isimujamii. Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili.
Msanjila,Y.P,
Kihore,Y.M na D.P.B Massamba (2011). Isimujamii sekondari na vyuo.
Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Samson,
H.R (1988). Ufundi wa magari, mfano wa ukuzaji wa istilahi za Kiswahili
katika
Mulika na.21. Dar es salaam. Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili.
Sewangi,S.S
(2004). Maana katika uundaji wa istilahi katika Sewangi,pdf.
Tumb-Masabo,Z.N.Z
na Mwansoko,H.J.M (2008). Kiongozi cha uundaji istilahi za Kiswahili.
Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
----------------------------------------------------------------------------------------------------------------
[ IJUE TEHAMA ][ KISWAHILI NA TEHAMA ]
___________________________________________________________________________________
[ IJUE TEHAMA ][ KISWAHILI NA TEHAMA ]